Pages

NASH MC.

Friday, May 1, 2015

KISWAHILI NA SANAA – MZIMU WA SHAABAN ROBERT.



KISWAHILI NA SANAA – MZIMU WA SHAABAN ROBERT.

Imetayarishwa na Abdul Rutona.

Kwa mujibu wa “Kamusi ya Kiswahili Sanifu”, Toleo la Pili: Lugha ni mpangilio wa sauti na maneno unaoleta maana ambao hutumiwa na watu wa taifa au kundi fulani kwa ajili ya kuwasiliana. Katika Makala yenye kichwa cha “Matumizi ya Lugha ya Kiswahili Katika Kazi za Sanaa” iliyoandikwa na Bwana  Khadil Kantangayo katika Blogu yake Tarehe 13, Aprili ya mwaka 2011, Mwandishi anaelezea kuwa  lugha ni mfumo maalumu wa sauti nasibu za kusemwa unaotumika na jamii ya utamaduni fulani kwa ajili ya mawasiliano au kupashana habari. Anaendelea kuwa  lugha zote duniani zina tabia zinazofanana ingawa sababu hiyo haifanyi lugha zote kufanana japokuwa kuna zinazokaribiana. Anaongezea kuwa lugha huathiriwa na lugha nyingine, na kuwa  lugha huweza kuongeza msamiati na mara nyingine huweza kufifisha msamiati na ukatoweka katika matumizi. Anamalizia kwa kusema kuwa  hakuna lugha bora kuliko nyingine, kila lugha ni bora kwa kuwa inakidhi haja ya mawasiliano.

Ninaungana na wale waaminio kuwa mafanikio makubwa yanayopatikana katika ujenzi wa utamaduni na utambulisho wa nchi yoyote ni lugha. Kwa Mtanzania, lugha hiyo ni Kiswahili…ambayo imetuunganisha wote na kutupa sifa moja muhimu ya UTAIFA.
Mwandishi hakuishia hapo, anajaribu kuelezea Sanaa kwa ufupi kuwa Sanaa ni ufundi wa kuwasilisha hisia na mawazo ya binadamu kwa mdomo, maandishi, michoro na uchongaji. Anaelezea  sanaa ya maandishi kwamba imegawanyika katika tanzu kuu tatu ambazo ni Tamthiliya, Riwaya na Ushairi na kwamba tanzu hizo zina vipengele vidogovidogo. Sanaa ya uchoraji, Sanaa ya uchongaji  na Sanaa ya Jukwaani na kwamba Sanaa za jukwaani ni sanaa ambazo hujumuisha nyimbo za miziki, maigizo na ngoma za kienyeji na kusisitiza kuwa  lengo likiwa ni kufikisha ujumbe kwa jamii.

Kwa upande wangu, nitajaribu kuelezea kwa ufupi sanaa hiyo ya jukwaani hasa katika nyimbo inavyoweza kutumika kufikisha ujumbe kwa kutumia Kiswahili. Nitatumia Santuri ya “Mzimu wa Shaaban Robert” ya Msanii “NASH EMCEE” ambayo ni moja kati ya dira makini zenye kila aina ya uono na fikra pevu katika kukuza na kuendeleza utamaduni wa lugha yetu aushi ya Kiswahili. Santuri hii inakusanya vibao 18, japo ni ina muda wa miaka kadhaa tangu ilipoanza kuuzwa, ujumbe upatikanao humo ni endelevu.


Nitajaribu kuelezea kwa kifupi kibao ambacho ni namba moja katika mpangilio wa vibao hivyo 18. Kibao hicho kinaitwa “MZIMU WA SHAABAN ROBERT”. Kibao hichi kilitayarishwa na Mtayarishaji “ABBY” pale “Tattoo records”.
Msanii kwa kuwa ni mwanaharakati wa lugha ya Kiswahili alitumia sanaa ya kujiita Mzimu wa Shaaban Robert kuelezea historia ya mmoja kati wa  washairi bora kabisa kupata kutokea barani Afrika. Msanii anaanza kuwaandaa waandishi kuwa wajiandae kuandika habari za mshairi huyo aliyezaliwa Tarehe 1 Januari 1909 kijiji cha “VIBAMBANI jirani na MACHUI kilomita 10 kusini mwa mji wa “Tanga” na kwamba alipata elimu yake katika Shule ya Msimbazi, jijini Dar-es-salaam kati ya miaka 1922 na 1926 alifaulu na kupata cheti cha kuridhisha na baadae kufanya kazi kwenye Mji wa “Pangani” (Aliajiriwa na serikali ya kikoloni kama karani katika idara ya forodha huko  mwaka 1926 – 1944. Bila shaka kukaa kwake miaka mingi katika mji wa kihistoria uliokuwa mahali pa utamaduni wa Kiswahili tena mahali patulivu kulisaidia maendeleo yake Shaaban kama mwandishi wa Kiswahili.).
Msanii anaendelea kumwelezea Mshairi Shaaban Robert kwamba alifanikiwa kuandika vitabu ishirini na mbili. Baadhi ya vitabu ni: Adili na Nduguze, Kusadikika, Kufikirika, Wasifu wa Siti Binti Saad, Baada ya Miaka Hamsini, na Maisha Yangu. Vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha za Kichina, Kiingereza na Kirusi na kuwa alifariki  huko Tanga Tarehe ya 22 Juni 1962, na akazikwa  huko Machui.

Kwa mambo makubwa aliyowahi kufanya katika maisha yake, alitunza kwa zawadi ya waandishi inayoitwa ‘Margaret Wrong Memorial Prize’na  pia aliwahi-tunzwa nishani ya M.B.E. Hakika alikuwa ni BABA WA KISWAHILI.
Msanii amejitahidi kutumia lugha ya Kiswahili katika vibao vyote 18 bila kuchanganya na lugha za kigeni hasa Kiingereza (labda kwenye maneno machache aliyolazimika kuyatumia na ni yale maneno yanayotumika sana amabayo hata mtaani nirahisi kueleweka). Natoa kongole katika hili..
Kwako NASH EMCEE, Kwa Baraka na dua zote, naamini utaendelea kufanikiwa katika kukuza na kuendeleza lugha yetu ya Kiswahili.

# Fikra_sahihi_huja_kwa_lugha_ya_asili.

Tuesday, April 21, 2015

HAKIKA "BAADA YA CHUO" HUAKISI MAISHA YA WASOMI WENGI.

Amani iwe kwenu mashabiki wakweli wa Nash Mc, leo kutoka katika maktaba yetu tumewaletea kile tukiaminicho kuwa Hiphop ni utamaduni ugusao maisha ya mwanadamu na ulikuja kumtetea au kumsemea shida zake ila pia  katika kipengele cha kazi ya fasihi (muziki) utamaduni huu bila huwa ni akiso la jamii.

Naam ni sahihi, ila mzuka unapanda pale tu kinapomaliza kibao nambari tatu (03) katika santuri kali ya MCHOCHEZI kilichotayarishwa na TROO akiwa ni miongoni mwa watayarishaji mahiri wa muziki (Hiphop), oi, baada ya kibao hicho kibao nambari 04 kinaingia kikiwa na jina la BAADA YA CHUO nacho kimetayarishwa na TROO naamua kukisikiliza kwa makini ndipo nikagundua " "HAKIKA BAADA YA CHUO HUAKISI MAISHA WA WASOMI WENGI".

Kwani ni pale tu mshairi (Nash Mc) anapojaribu gusia hisia, mawazo na maisha halisi ya wasomi nchini Tanzania pengine na kwingineko duniani, akielezea maisha ya wasomi waliopo vyuoni na wale waliopo mtaani wakiwa hawana ajira na changamoto za maisha wazipatazo, embu ona.

Ubeti wa kwanza:
Unaelezea mwanzo wa masomo kwa wanafunzi wa vyuo ukihusisha suala la fedha kwa ajili ya kujikumu (boom) hasa kwa wale wenye nayo wasiokuwanayo hivyo kupelekea baadhi yao "kula mara moja kwa siku"  kwani hawakuwa na kitu hasa boom lilipochelewa, hivyo kupelekea watoto wa kike kujiuza kila kona ili wapate pesa ya kutumia ndipo hapo sasa "ukistahajabu ya mimba utayaona ya ngoma".

Pia kutokana na kukosa fedha hivyo mawazo kuwafanya wanafunzi wengi wafeli masomo yao (kupata sup) na kuwataka warudi mapema vyuoni kurekebisha, lakini wapo waliodisco kabisa. Ingawa wanapitia hali zote hizo hatimaye msanii anawaambia.

... Sasa umemaliza chuo karibu nyumbani,
 Wenzio mwaka wa tano bado tupo maskani,
Tuna shahada mbili moja ya darasani,
Ya pili ya mtaani tunaishi kwa imani,
Tumedharaulika mpaka tumezoea,
Hatujapata kazi na umri unasogea,
Kumbuka elimu ya huku darasa ndiyo mtaa,
Wahadhiri walimwengu hakuna chakushanga,
Ukiwavunjia heshima haraka unageuzwa chengu,
Mtaa una elimu kubwa zaidi ya kule chuoni uliposoma,
Kwakuwa umesharudi  mwenyewe utayaona/

Ndiyo, ndiyo hii ni Hiphop iakisiyo jamii kwani katika jamii zetu sisi wenyewe tumekuwa mashuhuda wa hiki ambacho msanii amekighani katika kemo zake mahiri kabisa ila sasa uhondo unapatikana zaidi katika ubeti wa pili ambapo msanii anazungumzia maneno ya walimwengu kwa wale waliohitimu na wamerudi mtaani pamoja na harakati zao za kutafuta kazi na changamoto zingine nyingi.

Ubeti wa pili: 
Dharau na kejeli watu watakuponda,
Yule hana kazi kafeli kashaboronga,
Hawajaona vyeti vyako lakini bado watachonga,
Hao ndio waliomwengu usipowajua mawazo yatakuzonga,
Utajikuta unakonda unapaswa kujifunza wala usipagawe,
Mti wenye matunda ndo hupigwa mawe,
Fanya utakalofanya kwao hakuna la maana,
Zaidi ya kuonekana unajifanya msomi.
Wengine chuki zao wameziweka rohoni,
Wanasubiri wakosee wakutemee poo mate usoni,
Poleni wanazuoni,
Unaomba sana kazi kila siku unadunda,
Kaka hauna mavumba, 
Wewe na vyeti vyako ofisi zote za mjini umeshavuruga,
Kila fomu ya maombi imeandikwa kwenye mabano,
Mwombaji awe na sifa ya uzoefu (uzoefu gani) wa miaka mitano,
Ndo namaliza chuo naupata wapi uzoefu kwa mfano,
Kampuni kibao C.V umeshapeleka zikaeleweka,
Lakini mpaka leo hujaitwa kwenye usahili kisa hauna refa,
Rushwa ya ngono ndo hapo inaingia dada zangu wanaachia,
Mtoto wakiume unacho cha kutumia au ndo uchumi unao halafu unaukalia,
Mawazo ya kurogwa pia yatakujia, inabdi kuvumilia,
Usikate tamaa kitivo cha mtaa ndo hiki unapitia,
Na hizi ndo elimu ambazo nilikwambia,
Maisha baada ya chuo unaweza ukajifukia/.

Kwa ufasaha kabisa msanii anaifikishia jamii yake changamoto zinazowakabili kila siku katika jamii zao hasa ukosefu wa ajira na mwishoni anawapa ushauri, na kwa uwazi kabisa katika jicho la kichambuzi utagundua yote haya yanatokana na umasikini katika jamii zetu, uongozi mbovu n.k, hivyo kupitia wimbo huu jamii inabidi ipambane kujiletea maendeleo yake kwa kufa na kupona.

Mishororo ya ubeti huu wa mwisho umejawa ukweli mtupu (unahakisi) wa maisha ya wanafunzi wengi wa vyuo na maisha yao pindi wafikapo mtaani baada ya kuhitumu, ingawa hukutana na changamoto nyingi na nyingine zisizovumilika msanii (Nash Mc) anawapa moyo na ushauri kuwa "watu kusema ni kazi yao ... na waungwana husema namwachia Mungu, hivyo yote hayo wamwachie Muumba wa mbingu na ardhi (Mungu).

Angalia: Kibao nambari 04.






+255 (0) 654 30 40 30, Mwanazuoni (Mhariri andiko).
 






Wednesday, April 15, 2015

NASH MC: AJA TENA NA PICHA JONGEFU YA WIMBO " HASI 15 ".


Katika kuendeleza gurudumu la muziki wa Hiphop nchini Tanzania Nash Mc yupo katika ufanyaji wa picha jongefu (video) ya wimbo wake uitwao "Hasi 15" , ambao unaambatana sambamba na Ziara ya Kinasa, je, unajua kwanini "Hasi 15" ?, Nash Mc ametuachia hesabu hii 2000 -2015= -15, hivyo shabiki umiza kichwa, hii ndiyo sanaa ikiambatana na ubunifu wenye taharuki ndani yake. Kaa mkao wa kula.
Nash Mc.

NASH MC: "ZIARA YA KINASA BADO INAENDELEA".

Nash Mc rakabu Zuzu au Maalim Nash ni miongoni mwa wachenguaji mahiri sana nchini Tanzania akiwakilisha sanaa ya muziki kupitia ghani au kemo zake katika utamaduni wa Hiphop, kwa muda mrefu amekuwa ni mtu asiyekata tamaa katika sanaa yake kutokana na vikwazo mbalimbali akutanavyo ambavyo mara nyingi vimekuwa vikimjenga kiubunifu na kufanya makundi mengi kama vijana, wazee, wanawake katika nyadhifa mbalimbali kumpenda na kumuunga mkono katika ununuzi wa kazi zake.

Nash Mc alifanikiwa kufanya onyesho moja jijini Dar es Salaam na kufana vyema, onyesho lilijumuisha wasanii wengi wakiwemo P the Mc, Zaiid na wengine wengi toka jijini hapo vilevile ili kukamilisha maudhui ya tumbuizo hilo " KINASA# NashMcTemekeShow " alikuwepo Mzee. One Sigala toka BAKITA pamoja na waalikwa mbalimbali waliohudhuria siku hiyo.

Ilikuwa ni tukio la aina yake kwa wale walioweza fika kuunga mkono harakati hiyo, ziara ya KINASA bado inaendelea kwa maandalizi ya maonesho mengine mengi nchini Tanzania, ila unajua nini maana ya KINASA?,hujachelewa wewe mpenda sanaa, mpenda Hiphop, shabiki nambari moja wa Nash Mc, Santuri ya onesho lililopita imeshatoka pata nakala yako kuunga mkono harakati. Piga nambari zifuatazo kwa mahitaji +255 713 900 994 au +756 522 346. Amani kwenu.

Sunday, September 7, 2014

UNAKIJUA KIBAO CHA " MSHAIRI " KUTOKA KATIKA EP YA MCHOCHEZI ?


JE! UNAKIJUA KIBAO CHA " MSHAIRI " KUTOKA KATIKA EP YA MCHOCHEZI ?

Karibuni wapenzi wafuatiliaji wa blogu hii makini kabisa, leo kuna swali juu yako wewe shabiki wa Nash Mc, swali kama linavyosomeka hapo juu, je unamfahamu vipi NASH MC?, je unaelewa mapito ya kimaisha aliyopitia?, sasa nakuibia siri kuwa kibao nambari 03 ndiyo jibu.

Fanya hivi sikiliza kibao hiko utagundua mengi juu yake,   pata nakala yako ya MCHOCHEZI, sikiliza kibao kiitwacho mshairi, lakini ziada ni kuwa elimu, burudani kutoka vibao vingine vitakupa ile dhima ya kazi ya sanaa. sasa je, " hakuna anayetudai, sasa kwanini tusifurahiiii? ".


Na, Mwanazuoni (Mlela)/ Muendesha blogu

Saturday, September 6, 2014

# NashMC TEMEKESHOW Inakaribia......

.... Oi oi oi, wahenga husema saa hutengeneza siku, mwezi, hata mwaka. Kwa hisani ya HIPHOP, Nash Mc rakabu ZUZU, MCHOCHEZI, CHIZI, MAALIM na majina kibao katika uchenguaji wake, anawaletea tumbuizo wakazi wa Temeke na Dar es Salaam kwa ujumla.

Baada ya kikosi kizima cha maandalizi ya Show hiyo kujipanga vyema, kinawakumbusha mashabiki wa kweli kukaa mkao wa kufurahi siku ya tumbuizo hilo mara tu tarehe na siku vikitajwa, wewe na yule hamtakiwi kukosa siku hiyo.



                                             # NashMcTemekeShow  inakaribia.....

Saturday, March 8, 2014

NASH MC ATOA TAARIFA KWA UMMA: KUHUSU SANAA NCHINI NA HALI HALISI YA MAPOKEO YA KIBAO "KAKA SUMA".

TAARIFA KWA UMMA:Ilikuwa ni siku ya tarehe 7 - 3 - 2014, ambapo katika kurasa pembuzi za mitandao mbalimbali, na taarifa za habari toka vituo mbalimbali vya matangazo nchini Tanzania, ilisikika kuwa "mamlaka ya mawasiliano nchini (TCRA) imetoa onyo kwa kituo cha Redio Free Afrca (RFA) baada ya kuwa wamecheza wimbo wa msanii Nash Mc uitwao "KAKA SUMA", wakidai kuwa ni kinyume cha sheria za utangazaji na kwamba kufanya hivyo ni "UCHOCHEZI" uliofanywa na redio hiyo.
Taarifa ambazo Nash Mc alizopokea na hatimaye akapata wasaa wa kusema haya yafutayo;
"Binafsi naendelea kusikitishwa na mambo mengi hapa nchini, likiwemo na hili la TCRA.Wimbo huo uliotoka mwaka jana kati ya mwezi wa 6 na wa 7, ulichezwa katika vituo mbalimbali vya redio nchini na umefikisha ujumbe kwa 100% pasi na shaka, kuendelea kutujengea hofu kwa kusema ukweli ndio chanzo cha uvunjifu wa amani. Ikumbukwe kuwa kila mtu ana uhuru wa kutoa na kupokea habari bila ya kuingiliwa kwa mujibu wa katiba ya sasa, na ndiyo maana vyombo vya habari vinanyimwa uhuru kwa mchakato wa sasa wa kuelekea kupata katiba mpya. Nawakumbusha ,hii ni sanaa na ndio kazi kubwa ya "HIP HOP" na ndio njia sahihi ya kufikisha ujumbe kwa jamii sasa nashangazwa na sentesi ya uvunjifu wa amani.
Ukweli siku zote una nguvu na unapingwa vikali. Yanayoendelea bungeni ni udumishaji wa amani?.Mafisadi wanaokamatwa ni udumishaji wa amani?. Mauwaji ya tembo na biashara za dawa za kulevya zinazohusisha vigogo ni udumishaji wa amani?. Je ni kweli hakuna nyimbo zinazochochea mambo maovu na mabaya nchini zaidi ya KAKA SUMA?. Bora kufa umesimama kuliko kuishi kwa kupiga magoti. Nasubiri kusikia tena wimbo wa Nash Mc uitwao "NAANDIKA" ukifungiwa pia. Wabillahi Tawfiq!".
Hii ni kauli ya msanii Nash Mc, kama alivyotoa taarifa kwa umma (mashabiki wake) kuhusu kufungiwa kuchezwa kwa kibao chake, kwa tuhuma za kuwa kinachochea uvunjifu wa amani, lakini mashabiki, wataalamu wa sanaa, wanataaluma mbalimbali wanabaki wakihoji suala la kufungiwa kwa kibao hiki kuwa wamezingatia vigezo gani, na kuacha maswali kadhaa ikiwemo. 1. Je, mamlaka inatambua ni ipi dhima ya fasihi/sanaa katika jamii.
2. Wanahakiki kazi za msanii kwa kutumia vigezo gani?.
3.Je, katiba imefuatwa vyema hapo?, hasa ile ibara ya 18, SURA YA KWANZA, SEHEMU YA TATU?.
Hayo ni baadhi ya maswali toka kwa wataalamu wa sanaa, mashabiki n.k, sasa ni jukumu lako shabiki kutafuta kibao hiko na kukipitia kwa jicho la kihakiki, ili ubaini kinachoongelewa, , upendo mmoja, amani itawale, AKHSANTE
Mwanazuoni, 2014 (muendesha blogu).

Monday, March 3, 2014

BAADA YA "NAANDIKA" SASA NASH EMCEE AJIAANDAA TOKA NA "EP".

Oi, oi, oi, kama ilivyoada utamaduni wa Hiphop unavyotulea katika misingi yake ELIMU NA BURUDANI, basi nasi hatuna budi kutomuangusha mlezi huyu, leo katika blogu letu makini kabisa, kuna hili, NASH MC, baada ya kuachia kibao chake "naandika",mwanzoni mwa mwaka huu na kupokelewa vizuri na wanajamii (Wapenzi wa HipHop.
Sasa yuko jikoni akijiandaa kutoka na "EP", yaani "Extended Play", mmmh!, " EP", ndo, nini sasa?, waweza jiuliza ukabaki na uvulivuli katika hili, ila hapa tutaelezana, dhana hii inanikumbusha kipindi THORIA alivyoachia kazi zake zake za mwanzo kabisa katika mfumo huu, hivyo sasa "EP", ni demo album (santuri) yenye nusu nyimbo zitakazokua kwenye album(santuri) ni kama
trailor tracks (vionjo) vya albam inayokuja, wakati mwingine watu wanatoa ili wawape mashabiki kitu cha kuwa weka katika umakini kabla album (santuri) kamili haijatoka, na inakuwa na nyimbo mpaka 7, hivyo sasa Nash anawaambia mashabiki wake wakae mkao wa kupata kazi hii, endelea kutembelea www.nasheemcee.blogspt.com, waambie na wale pia, HipHop Kwa Maisha.

Thursday, February 20, 2014

" NAANDIKA ", NI KIBAO KIPYA CHA HIPHOP MWANZONI MWA 2014, JE WAJUA KIMEBEBA MAUDHUI YAPI?, FUATILIA HAPA UJIFUNZE.

NASH MC kwanini kaandika, na kuna nini kwenye "NAANDIKA"?.
Salamu kwanza kwa kila mmoja, naam!, naimani kila mmoja yu salama, na anaendelea vyema na shughuli za ujenzi taifa, na kwa wasio vyema kiafya na mengine Mola awape shifaa katika hilo.
HIPHOP, ndiyo kitu nachogusia hapa kwa maana ya wasanii wake (watu waishio ndaniye), au jamii nzima, lakini mguso wangu ulipewa nguvu zaidi pale nilipotumiwa wimbo huu "NAANDIKA" na leo nilipoupakua ili nipate ukiwa na kiwango bora zaidi (high quality mp3) kwa maana wakwanza ulitumwa kwa whatsapp.
Lakini pia kama ilivyo ada huwa na kitabia cha kupitia hapa na pale hili kupata kiduchu kuhusu utamaduni huu wa hiphop au sanaa kwa ujumla hivyo safari yangu ikapitia hapa, Hanzi, M.S, (2012), Chuo Kikuu cha HipHop, Ubunifu Wetu Printing Press, Dar es Salaam: Tanzania, katika kurasa kama nambari 15, na nyingine kadhaa, ndipo nkagundua kuwa mwandishi kakumbusha kuwa HIPHOP NI MAARIFA, pia aligusia nguzo za hiphop hapo miye nkajikita elewa maarifa kama nguzo ya utamaduni huu.
Yote hayo, nkaja yaweka katika uchambuzi huu wa wimbo "NAANDIKA", toka kwa NASH MC, kama msanii wa HIPHOP niligundua kuwa katika NGUZO YA MAARIFA imesawiriwa vyema naye, kwani MWANAHIPHOP yoyote anakumbushwa kufuatilia mengi katika jamii, kusoma ili aweze kuwa na uelewa mpana yaani asiwe nyuma (ajisasishe).
Hivyo sasa, Nash Mc katika kibao hiki kupitia ghani zake kaongelea mengi yatokeayo duniani (jamii), ambayo pengine ukiyasikiza vyema waweza pata jambo na kugundua vitu vitakavyoleta mabadiliko, wimbo huu kwa upande wa fani msanii ameonesha falsafa yake ambayo ni mapinduzi katika fikra za wengi jamiini kwa mtindo ninaoweza uita ghani yenye mlengo kumbushi,ambayo imechokoa mambo bila kutoa masuluhisho ya jumla, kwa maudhui kuna pipa la dhamira ambacho ndiyo lengo la maandishi haya.
Msanii anaonesha haya yafuatayo. 1. Suala la imani (ya kidini), kuwa yeye kama msanii anapaswa/ anaandika kuhusu utukufu wa Mungu wake, ambaye ndiye anamuongoza kwenye maisha yake, na si mwingine yeyote, hivyo hili ni kama kumbusho kwa wanajamii wamuamiao Mungu kumkumbuka na kumtukuza (hasa wasanii), wasiandike raha tu (starehe) na kumsahau yeye, rejea ubeti wa kwanza anaposema "naandika kuhusu utukufu wa mungu wangu, anayeniongoza kwenye haya maisha yangu/''.
2.Suala la mapenzi ya dhati ya utamaduni. Msanii nash Mc anaonekana ni mtu mwenye mapenzi ya dhati ya utamaduni wa HIPHOP na abadani hakubali utamaduni huu upotee kizembe kwa kupotoshwa, hili laonekana pale aliposema "bila kusahau utamaduni wa HIPHOP naipenda hii kitu, hivyo sasa kuacha jambo kwa wapenzi wa utamaduni huu kuupenda vilivyo utamaduni huu kwa kuunga mkono harakati, kazi za wasanii wake.
Pia msanii anaendelea dodosa mengi zaidi pale anapoonesha yatokeayo Afrika na nyumbani pia (Tanzania), mfano. 3.Suala la vita vya wenyewe kwa wenyewe (Afrika ya Kati, Kongo na Sudan). Kweli kakumbusha jambo adhimu linalopaswa kuandikwa na Wasanii hasa wa HIPHOP ambao ndio utamaduni KOMBOZI WA JAMII, na kuacha kuandika kuhusu bifu, katika hili msanii anaonesha athari za vita hivyo kama mauaji ya akina mama na watoto, udhalilishaji wa wanadamu, ikiwa ni athari ya vita, msanii kakumbusha kuwa "naandika", kama kichokoo cha kila mwanahiphop kugusia haya, naandika kuhusu.
4.Kupanda kwa gharama za maji na umeme. Kwa watu wa majumbani ambao ndiyo wengi nchini Tanzania wenye kipato cha chini na maisha yao ni magumu hivyo hili ni kama gharika (TSUNAMI), hapa anakumbusha serikali iliangalie hili kwani ni mwimba kwa jamii hiyo yenye hali chini.(rejea kibao hiko).
5.Suala la kukosa uzalendo, dili za magendo, uuzaji wa pembe ze tembo. Yote haya mwandishi ANAANDIKA na kujaribu chokoza hisia za wasikilizaji wake pengine kuwafumbua macho kuhusu hali ilivyo nchini kwetu pengine Afrika, ambapo wananchi na viongozi wanakosa uzalendo juu ya mali zao, pengine ndipo panapopelekea dili za magendo na mauaji ya tembo kwa watu wachache na kuhujumu rasirimali taifa.
6.Kutokuwepo na mgawanyo sahihi wa keki ya taifa (utabaka)/ faida-rasirimali. Hapa navuta hisia zangu katika haya yatokeayo Afrika hasa huko Kongo, Afrika ya Kati, Sudan ambapo mapigano yao kwa asilimia kadhaa chanzo chake ni rasilimali zilizopo, lkn pia tukumbuke yale yaliyotokea Mtwara (sakata la gesi), je vipi kuhusu ule mgogoro wa ardhi (wafugaji na wakulima) huko Morogoro, ndipo msanii akasema "naandika" kuhusu gesi, mbuga, ardhi na madini kama vitu muhimu ambavyo mara nyingi siku hizi wanapewa watu wenye mifuko mizito (wawekezaji) na kuacha wazawa wakilia na kunyanyasika, (rejea maeneo yenye migodi na athari zake).
7.Suala la kupotea kwa vijana katika mitaa (wavulana kwa wasichana). Ambao ndiyo nguvu kazi kwa jamii, mfano.pale anapoghani " njoo kwenye mitaa vijana wamepotea vibaya, dada zetu wamekuwa malaya/", kwa msongo wa mawazo wanatenda mabaya/, mpaka wanasahau kuhusu dhambi wao pombe na khaya, hivyo mwandishi anagusia kuhusu kuacha hayo mambo maana ni hatari., kwakweli NAANDIKA imeonesha mengi embu ona haya pia. 8.Athari za ngono isiyo salama, inayomaliza kundi kubwa la vijana. 9.Wasanii kutotunga kazi zinazohamasisha ngono za jinsia moja, na kumkumbusha Rais kuwa akitia sahihi yeye ni muoga (kwa kutokuwa na msimamo wake), hivyo asikubali mashinikizo ya mataifa ya magharibi.
10.Kutokubadilika kifasalfa (kama msanii), kwa minajiri ya kupata muda wa kusikika hewani ili upate mafanikio ilhali unaandika vitu visomaana katika jamii mfano. kuwepo kwa ghala kubwa la nyimbo za mapenzi kila kukicha wakati jamii ina mambo mengi ya kuzungumzia mf. anasema " Unaandika kuhusu mapenzi hiyo ni kwa hisani ya radio fulani, jambo ambalo linawarudisha wasanii utumwani (kwa kuwanyenyekea watangazaji, wadundishaji wapige kazi zao), Pia anasisitiza.
11.Matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye fani ya ushairi. Kama muega mmoja wapo wa uzalendo na kufanya kazi zetu zikubalike mbali kwa kupenda vyetu, na kuacha ule utumwa kuwa ukighani au imba kingereza ndiyo mjuvi sana, hivyo kuonesha kuwa huo ni ubunifu tu katika lugha japo si lazima sana, kwani msanii anaamini " kuwa fikra sahihi huja kwa lugha asili" nayo ni Kiswahili.
12.Kutobadilika kutoka kule ulikokuwa (HIPHOP), na kwenda katika baibuda kiduku, kwaito kisa mafanikio ya haraka, hii si sawa kwa mwana hiphop halisi, kwani jamii inatakiwa ifahamu kuwa "nakala mia moja za HIPHOP ni bora kuliko nakala 1000 za muziki mwingine, usiozungumzia jamii na ukweli (ukombozi).
13.Kuwepo kwa watangazaji na wadundishaji wala rushwa. Msanii anawakumbusha hao kuwa "wasiombe kukutwa na takukuru ya mtaa.
Kwa ujumla msanii NASH MC kazungumzia mengi katika kibao hiki katika aina ya ghani ya kunata juu ya mdundo mahiri, katika mtindo wa kukumbusha jamii, juu ya mambo mbalimbali yanayoikabili, na kuwachokoa wasanii wengine wa Hip Hop "waandike" juu ya haya aliyoyandondoa kibaoni humo, naam!!, haya ndiyo maarifa na hii ndiyo nguzo mhimili katika hiphop, utamaduni adhimu kabisa, tafuta kibao hiko ujikumbushe mengi.
Mwanazuoni, 0654 30 40 30.

Wednesday, February 19, 2014

P THE MC NA " BORN TO RHYME NOT TO SHINE "..

(Knowledge), ni mhimili mkuu katika utamaduni wa " HIPHOP " ambao huwaongoza wasanii wafanyao/ waishio katika Utamaduni huu kuwa wabunifu katika kazi za mikono yao, naam!, nguzo hiyo pia imetumiwa vyema na MC huyu toka Kiwalani Bom Bronx au TAMADUNIMUZIK, naam huyu si mwingine bali ni P THE MC ambaye leo katokea bloguni humu, karibu mpenzi wa HipHop tujumuike. " P the Mc "
" toka TAMADUNIMUZIK,ameingiza sokoni mzigo wa "Fulana" (T-shirts) halisi kabisa, kila rangi na kila ukubwa (size), kwa bei ya fedha halali ya Kitanzania sh. 15000./= tu, hivyo mdau wa sanaa ni wakati wako sasa kuunga mkono harakati hizi, pendeza katika "fulana" za kijanja kabisa zenye nembo (LOGO) isomekayo "BORN TO RHYME NOT TO SHINE" au "MWINGI WA HABARI". Ili kupata mzigo wako, fika Kilingeni Msasani Club ni Kila Jumamosi, au piga simu nambari hii: +255 717 254 451.

YARUDI UPYA KWA MAARIFA KUHUSU HIPHOP, BIDHAA ZA WASANII WA HIPHOP, MAKALA/ CHAMBUZI MAKINI .

, Baada ya ukimya mrefu kiasi sasa blogu hii yaanza rasmi kuwaleteeni habari kuhusu wasanii wa HipHop Tanzania, Harakati zao, bidhaa zao mfano (santuri (albums), kandamseto (mixtapes), fulana zao
(t-shirts), mashairi ya tungo zao (lyrics), makala elimishi, chambuzi makini za
kazi zao za sanaa n.k, ushirikiano wako ni muhimu katika kutoa maoni juu ya kile tunaweka yaani pachiko
zetu (posts), mwambie mpenda HIPHOP yeyote wakweli juu ya hili, HABARI IFIKE MBALI.

Tuesday, September 24, 2013

KWANINI NASH ALIJIITA ''MC''?,NANI ''MC'' WA KWANZA,NA NI NANI ALIANZA TUMIA NENO ''MC'' KATIKA HIPHOP?
Naam! sikufikiri na sikudhani kama nilikuwa mwenye makosa makubwa pale nilipokumbuka kuwa mimi ni miongoni mwa watu wenye kuutakia mema utamaduni huu wa HIPHOP kila kukicha kwa kadri nilivyojaaliwa,lakini kutokujuta kwangu moja kwa moja nikiwa nimejiegesha katika kikochi na sauti ya wastani ya ghani mahiri toka kwa wachenguaji bora walionifanya nigeuke teja wa kusikiliza iliingia katika ngoma za masikio yangu.
Vibao vyao na mitambao yao vyote viliendelea chakatwa na ubongo wangu vyema na moja kwa moja vikanisanisafirisha mpaka kwenye kitabu maridhawa kabisa kuhusu utamaduni huu wa HIPHOP nikapenyeza kidole na kwenda kubisha hodi kwenye ukurasa ulioandikwa yaliyomo nao moja kwa moja ukanielekeza ukurasa wa 47 ambapo nilijazwa unene wa maarifa nilipogundua kuwa kilichozungumzwa hapo ni NGUZO ZA HIPHOP,ambapo hapo wengi walijimwaya na kutaja idadi ya NGUZO ZA HIPHOP mfano,
TOVUTI YA URBAN DICTIONARY Ilitoa idadi ya nguzo kama tisa (9)kwa idadi yake kama Mcing,d-jaying,battlelling,graffiti,B-boying,Beat boxing,The style(fashion),The slang,rope skipping,pia hawa hawakubaki nyuma.
WIKIPEDIA. Mtandao huu ulitoa hizi Mcing,d-jaying,break dance,na graffiti,beat boxing,lakini katika hizi Mwanaharakati AFRIKA BAMBATAA alizitaja zote kasoro beat boxing,sasa nkajiuliza JE KUNA NGUZO NGAPI ZA UTAMADUNI HUU?
YOUTH ETHICS INITIATIVE INC kwa ushirikiano na CHUO KIKUU CHA MIAMI. Walisema kiasilia kulikuwa na nguzo nne (4) yaani Uchenguaji,umanju,uvunjaji,machata lakini nguzo ya tano ''Maarifa''ikaongezeka
Swadkta kabisa kuangalia muda nikiwa safari nilijikuta nkigonga mlango (ukurasa) nambari 48 palipodadavuvuliwa nguzo ya maarifa kwa heshima kabisa nikaisoma na kuhitimisha katika kutafuta mengi pitia vyanzo mbalimbali nikazidi ingia ndani ya milango hiyo nikajikuta nikigonga mlango nambari 54,56 na 58.na kuwaleteeni haya.
NANI ALIKUWA ''MC'' WA KWANZA? Ni swali zuri lakini wengi tunaopenda HipHop hatufahamu kama ni kweli,narudi palepele kwamba tafuta ufahamu/maarifa (Knowledge)kama mimi ninavyojaribu pindi panapopatikana upenyo ama muda,safi jibu la swali ni kwamba ingawa inaaminika kuwa COKE LA ROCK ndiye aliyekuwa mchenguaji wa kwanza wa HIPHOP lakini si wa kwanza kuanzisha neno ''MC''sasa.
JE NANI ALIANZA TUMIA NENO HIPHOP? Ndiyo,swali mezani kama tulivyoona hapo juu kuwa Bw.Coke La Rock ndiye mgahanaji wa kwanza lakini hakulitumia neno ''MC''katika kujiita na kuliingiza katika utamaduni wa HipHop kwa kina lakini MELLE MEL huyu anageuka kinara wakuliingiza neno hili katika Hiphop,ndugu huyu aliyezaliwa huko South Bronx jijini New York,Marekani mwaka 1961,alileta athari kubwa katika utamaduni wa HIPHOP kwa kuleta mitindo mbalimbali ya ghani,Mchenguaji wa HipHop wa kwanza kupata tunzo ya Grammy,pia kibao chake kiitwacho ''The Message'' ndicho cha kwanza katika utamaduni wa HipHop kuingia katika kumbukumbu za taifa za vibao vya kihistoria (United States National Archive of Historic Recordings),toka katika hili ndipo laja hili.
JE KWANINI NASH ALIJIITA ''MC''? Katika tafsiri zoefu neno ''Mc'' ni mchenguaji au mshereheshaji au kwa kimombo yaweza andikwa kama ''Master of ceremony''kwa maana ya kuwa muongoza hafla ama sherehe au tumbuizo,akhsante sidhani kama nimetukana katika hili lakini naamini kuwa majina yetu mengi tumerithi kwa wale tulowakuta kwa lengo la kuwaenzi au mapenzi yetu,hivyo kama mistari kadhaa hapo juu ilivyoeleza kuwa MELLE MEL ameacha athari ya mitambao mingi kwa wale waliomfatilia/mashabiki wake hivyo hata jina au neno ''MC'' limekuwa chachu kwa Wanahiphop wengi kujiita mfano,leo tuna NASH MC,P THE MC na wengine wengi pia,lakini athari hizi haziishii tu katika majina bali athari kwa Waghanaji wengi wanaomkubali na kumuelewa Melle Mel,mfano hapa.
Nash MC anasema ''Melle Mel ni mtu wa kwanza kudondosha mistari mitamu,ule utamu wa mistari umeanzia kwa huyu mtu''. Hivyo sasa nakumbuka usemi usemao mwisho wa kizuri cha leo ni mwanzo wa kizuri cha kesho,ndugu zangu katika utamaduni huu naomba niwaache mkiperuzi haa machache niliyowaandaleni,AMANI KWENU. (shukrani,(REJEA,Hanzi,M.S,Chuo Kikuu Cha HipHop(2012),Ubunifu Wetu Printing Press,Dar Es Salaam)uk,54,56 na 58. WAKO,Amri Mlela/Niite Maalim (0654 30 40 30).

Thursday, September 12, 2013

JE NASH EMCEE ANAIZUNGUMZIAJE MITINDO HURU?
Ndugu wadau,wakereketwa au wanunuzi wa kazi zetu za HIPHOP na wote wanaotoa mchango wa hali na mali katika kuhakikisha gurudumu la sanaa hii linateleza kama tutakavyoona inafaa..
Leo katika blogu yetu hii ndugu wasomaji na wadau wake tuna kijimada hapo kama kinavyosomeka hapo juu...
Nash Emcee alipata fursa ya kuzungumzia jambo hili ambalo limeonekana kukanganya mbongo za sisi wafatiliaji kwa kujua kuwa mitindo huru au FREE STYLES ni katika nguzo za HIPHOP hivyo sasa Nash anajaribu elezea suala hili kama inavyoonekana hapa chini,karibu....
"Bongo (Tanzania)watu wamejaribu kuingiza mitindo huru kama nguzo ya Hiphop,hakuna freestyle ''mitindo huru'' kama nguzo ya HipHop lazima uwe unajua kughani ndipo uweze kufanya mitindo huru,hiyo ni kama binzari (kinogeshaji)tu katika ughanaji"
Katika hali halisi tu,hakuna mtu yeyote ambaye anaweza kufanya mitindo huru ya HipHop bila kughani.Mitindo huru ni moja kati ya vipande/kijisehemu kinachounda nguzo ya ughanaji(EMCEEING)....
Ndugu msomaji katika hili na katika kile kinachosisitizwa kuwa Mwanahiphop anahitaji tafuta maarifa (knowledge) katika mambo mbalimbali yanayomzunguka hata pia katika utamaduni wake,natumai ntakua nimejaribu rahisiha hilo katika kupeana maarifa,Amani Kwenu.
(shukrani_(REJEA,Hanzi,M.S,Chuo Kikuu Cha HipHop(2012),Ubunifu Wetu Printing Press,Dar Es Salaam.

Monday, September 9, 2013

MHADHARA WA HIPHOP....MHADHARA WA HIP HOP....MHADHARA WA HIPHOP

Kwa wale wakazi wa Bandari ya Salama zamani kuitwa MZIZIMA Ni fursa yenu na hii si ya kukosa,lakini mtajiuliza ni nini hiki? Utamaduni huu umekuja kupeana elimu/maarifa (knowledge) hivyo hatuna budi peana chakula hiki cha akili,Sasa soma hapa chini upate maelekezo. TAREHE: 13/09/2013 MUDA: 11:00 - 1:00 JIONI WAPI: ALLIANCE FRANCAISE KIINGILIO: BURE KABISA Wadau,wakereketwa wa utamaduni huu wote mnakaribishwa siku hiyo njoo ujifunze mengi kupitia ''MHADHARA HURU'' utakaotolewa na NASH EMCEE (Maalim),bila ajizi siku hiyo atatukumbusha na kutuelezea ni nini *Machata,*Wachenguaji*Wadundishaji,*Mavunjaji*Maarifa kwa wenye vipaji,
Mwambie yule na wale pia...

JIFUNZE MENGI KUHUSU HIPHOP ---- kupitia blogu hii nashemcee.blogspot.com

HIPHOP umekuwa ni utamaduni au nyenzo adhimu kabisa ambao unawaunganisha watu wa aina mbalimbali hapa duniani hasa kwa wale wanaoishi katika misingi yake,kwani mbali na kuburudisha hadhira yake,umekuwa ni utamaduni wa kuyaangazia mambombali katika jamii zetu kwa jicho ang'avu lisilo na shaka na kujaribu kutoa suluhu au kuchokoa mambo mbalimbali na kuwaacha watu wakiwa katika tafakuri la kipi wakifanye baada ya kuupata ukweli kupitia HIPHOP,thibitisha hili kwa kurejelea kibao cha ''NASH MC'' Kaka Suma na vingine vingi adhimu. Kila kitu kizuri huwa na changamoto nyingi mfano.ni hili watu wanaojiita WANAHIPHOP kutojifunza zaidi na kufata misingi ya utamaduni huu,hivyo ni wajibu wetu kujifunza ukweli na undani wake,AKHSANTE.

Monday, March 25, 2013

SHOW YA LIVE HIP HOP TOKA KWA TAMADUNI MUZIK NI JUMAMOSI HII PALE NEW MSASANI CLUB KUANZIA SAA 11 JIONI.
KIINGILIO TSH. 5000/=

HIP HOP VYUONI.

TAZAMA BAADHI YA PICHA ZA MHADHARA WA ELIMU KUHUSU HISTORIA YA HIP HOP NA UHALISIA WAKE ULIOFANYIKA KATIKA CHUO KIKUU CHA DODOMA JANA (U DOM)..WATU WENGI WALIJITOKEZA NA ILIKUA NI SIKU YA HISTORIA SANA!! MHADHIRI NASHIR ALIKUA NA JUKUMU LA KUENDESHA MHADHARA HUO AMBAO ULICHUKUA ZAIDI YA SAA 4!! NITAPITA KILA CHUO KUHAKIKISHA ELIMU JUU YA UTAMADUNI WA HIP HOP UNASAMBAA IPASAVYO!! MUNGU TUBARIKI!!

Friday, December 7, 2012

UZINDUZI WA SANTURI NNE (04) KUTOKA TAMADUNIMUZIK.

Uzinduzi wa santuri nne (04) kutoka Tamadunimuzik mnamo tarehe 08/12/12 pale New Msasani Club kwa kiingilio cha elfu tano tu njoo upate raha ya HIP HOP kutoka Tamadunimuzik. Santuri ya KAD GO, AZMA, MANSU-LI, na MUJWAHUKI zitazinduliwa kwa pamoja. Karibu wewe mpenda HIP HOP uje uunge mkono na uendeleze harakati na mapinduzi ya HIP HOP.

Friday, November 30, 2012

UZINDUZI WA SANTURI NNE (04) KUTOKA TAMADUNIMUZIK

Tarehe 08/12/2012 kutakuwa na uzinduzi wa santuri nne kwa pamoja kutoka TAMADUNIMUZIK ndani ya #New Msasani Club kwa kiingilio cha shilingi elfu tano (5000/=) tu getini.
KINA KIREFU | TOLEO LA KWANZA LA MUJAHUKI | JOIN THE REVOLUTION | LOVE STORIES |. HII SIO YA KUKOSA MTAMADUNI NA MPENDA HIP HOP.